Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa katika eneo la Pwani wamehimizwa kufanya kampeni zao za kisiasa kwa njia ya amani na uiano ili kuwaunganisha wakenya.

Kulingana na Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mombasa Padri Wilbard Lagho, mara nyingi wakenya wengi huzozana kutokana na matamshi ya chuki na uchochezi yanayotolewa na viongozi wanaounga mkono hatua ambayo inafaa kusitishwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi Padri Lagho amesema kuwa itakuwa bora iwapo viongozi hao wa kisiasa wataiga mifano ya mataifa ya magharibu jinsi yanavyoendesha kampeni zao za kisiasa kwa utangamano, akisema kuwa hatua hiyo itaboresha usalama wa taifa hili.

“Tunawaomba viongozi wa kisiasa kufanya kampeni zao za kisiasa kwa njia ya amani na uiano ili kuwaunganisha wakenya pamoja na kuzuia kushughudiwa malumbano na migogoro inayosababishwa na siasa za chuki na uchochezi ili taifa hili na hususan eneo la Pwani kuwa salama,” alisema Lagho.

Kiongozi huyo wa dini ya kikristu amewashauri wakenya kuwachagua viongozi waadilifu na waajibikaji ili kuhakikisha kuwa masuala ya maendeleo, uchumi, usalama na uwekezaji unafakishwa.