Viongozi wa kisiasa nchini wameshtumiwa kwa kulichukulia swala la Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru kama la kisiasa, kikabila na kumkandamiza mwanamke.
Kulingana na Afisa mkuu wa Shirika la Maji na Ufasini eneo la Pwani Hamisa Zaja, viongozi wa kisiasa wamedhihirisha wazi kutowathamini viongozi wanawake kwani kulingana na jinsi kamati ya bunge kuhusu fedha ilivyomfanyia mahojiano waziri huyo wa ugatuzi. ilikiuka maadili na haki za wanawake nchini.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Zaja alisema kwamba viongozi wa kisiasa wanafaa kumchukulia waziri Waiguru kama viongozi wengine waliyokumbwa na kashfa za ufisadi na utaratibu uliofuatwa wakati huo ndio unaofaa kutumika na wala sio kumdhalilisha kiongozi mwanamke.
Wakati huo huo, alisema kwamba wangechukua utaratibu wa kuwasilisha kesi mahakamani iwapo viongozi hao hawana imani na Tume ya Maadili na Kupambana na ufisadi nchini EACC, kuliko kudunisha Waziri Waiguru kwa kuwa ni kiongozi mwanamke.
"Tungependa kuona utaratibu ufaao ukifuatwa kama vile mawaziri walioshutumiwa kwa kashfa za ufisadi walivyochukuliwa hatua. Kwa nini Ann Waiguru ndio anadunishwa kwa sababu yeye ni mwanamke? Hiyo ni kuwadhalilisha wanawake nchini na mimi kama mwanamke ningependa viongozi wafuate utaratibu sio kuwakandamiza wanawake,” alisema Zaja.
Haya yamejiri baada ya malumbano ya kisiasa baina ya viongozi wa mrengo wa Cord na Jubilee kuzuka wakimtaka Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru kujiuzulu kutokana na kashfa za ufisadi zinazomwandama baada ya kupotea kwa shilingi milioni 791 katika wizara yake.