Kufuatia tetesi kali kuibuliwa kuwa baadhi ya kanisa nchini zimekuwa zikuwatapeli wakenya pesa zao, sasa kiongozi mmoja wa kanisa la PAG amejitokeza kuitaka serikali ya kitaifa kuweka mikakati ya kuhakikisha wahubiri matapeli hawaruhusiwi kuhudumu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu katika kanisa ya Gesiaga siku ya Jumapili, mhubiri Denis Irani alisema kuwa badala ya serikali kupiga marufuku wahubiri kuitisha sadaka, inafaa itafute mbinu mwafaka ya kusuluhisha tatizo hilo. 

"Serikali inastahili kutafuta mbinu ya kuwahakikisha kuwa wahubiri matapeli hawaruhusiwi kuhudumu, badala yake kupiga marufuku kuitishwa kwa sadaka na wahaburi kupitia vyombo vya habari," alisema Irani. 

Irani aidha alisema kuwa kanisa zina mbinu ya kuadhibu wahubiri wanaowatapeli wakenya, huku akisisitiza kuwa wahubiri wana haki ya kuitisha sadaka kutoka kwa waumini, hali aliyosema huenda ikawalazimu wahubiri kuitisha maandamano iwapo serikali itashikilia msimamo wake wakupiga marufuku ukusanyaji sadaka. 

"Jukumu la kanisa ni kuhakikisha kuwa watu wanahubiri na kubadilisha maisha yao kwa kumrudia kristo, na kwa kweli sisi tutaendelea kuitisha sadaka kutoka kwa waumini, na iwapo serikali itashikilia msimamo wake wa kupiga marufuku hiyo, basi tutaandamana," aliongezea Irani.