Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nakuru imeteta vikali kutokana na hatua ya kubatilishwa kwa njia ambayo mradi wa reli wa SGR utapitia.

Viongozi hao wakiongozwa na Gavana Kinuthia Mbugua na Spika Susan Kihika wamesema kuwa hatua hiyo haikufaa kwani wengi hawatanufaika na mradi huo.

“Hata baada yetu kukaribisha hatua ya mradi huo kufikishwa hapa mjini Naivasha kwa awamu ya kwanza, kubatilishwa kwa njia hiyo huenda kukaadhiri uchumi wa mji huu,” Gavana Mbugua alisema.

Gavana huyo aliyasema haya katika eneo la Mai Mahiu siku ya Alhamisi baada kutembelea wafanyibiashara 21 ambao mali yao iliteketea wakati wa mkasa wa moto Jumapili iliyopita.

Familia hizo pia zimepata fidia ya shillingi laki moja kila mmoja kutoka kwa serikali hiyo.

“Tutapeleka lalama zetu kwa serikali ya kitaifa kuhusiana na kubadilishwa kwa barabara hiyo ya reli, Spika Kihika alisema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa muungano wa vijana wa kaunti ya Nakuru Charles Mburu alisema kuwa wakazi wote walifaa kubahatika na miradi inayofanyika eneo hilo ikiwemo ile ya mvuke.

Naye mwakilishi wa eneo hilo Stephen Ng’ethe alisema kuwa vijana wa sehemu hiyo ni sharti wapewe kazi pindi tu mradi wa ujenzi wa reli hiyo utakapoanza.