Viongozi waliochaguliwa katika nyadhifa mbalimbali za Chama cha ODM katika eneo bunge la Borabu wameonya vikali chama hicho dhidi ya kuwapokeza stakabadhi za kuwaidhinisha viongozi wasio na umaarufu mkubwa wakionya kuwa iwapo hilo litatokea pasina shaka wanachama wengi watalazima kuhama chamani.
Wakiongozwa na mwenyekiti mpya wa chama hicho tawi la Borabu Peter Manwa, viongozi hao walisema kuwa wapo tayari kuimarisha umaarufu wa chama hicho mashinani, akionya kuwa iwapo chama hicho kitapendea watu flani kwa kuwapa uteuzi wa moja kwa moja basi wanachama wa ODM watalazimika kukihama chama hicho mara moja.
"Sisi kama viongozi wa chama cha ODM tuko tayari kuuza sera za chama mashinani ilo kuhakikisha kuwa tunaimarisha umaarufu wa chama hiki, bali hilo tu litatokea iwapo viongozi wakuu wa chama hiki hawatawapendelea baadhi ya watu kwa kuwapa uteuzi wa moja kwa moja chamani," alionya Manwa.
Manwa aidha aliongeza kusema kuwa hulka za kuwapa uteuzi wa moja kwa moja wa watu fulani wanaopendelewa chamani imekuwa ikishuhudia katika maeneo mengi ya Gusii, hali aliyosema huwanyima nafasi wagombezi maarufu kupewa vyeti vya uteuzi wa moja kwa moja.
"Kwa niaba ya viongozi wenzangu, tuko tayari kuuza sera za chama mashinani na hata pia kuwasajili wanachama wapya chamani kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao ila tabia ya watu wasio na umaarufu mkubwa kupewa uteuzi wa moja kwa moja huwanyima nafasi viongozi shupavu kuongoza," aliongezea Manwa.
Viongozi hao aidha waliomba chama cha ODM kufanya uteuzi wa mapema chamani ili kuwapa nafasi wagombezi wa nyadhifa mbalimbali kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.