Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Uhasama na mvutano wa kisiasa kati ya serikali kuu na muungano wa Cord umetajwa kuwa chanzo kikuu cha masaibu yanaowazonga wakenya.

Kinara wa chama cha National Amani Congress Musalia Mudavadi ameyakashfu malumbano hayo na kusema kwamba yamemzonga mkenya ambaye anatarajia makubwa kutoka kwa viongozi wao.

Katika mkao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi baada ya kuzuru maeneo mbalimbali kukutana na wanachama wa chama hicho, Mudavadi alisema kwamba serikali inafaa kutimiza ahadi ilizotoa kwa wakenya wakati wa kampeni za uchagazi wa mwaka 2013.

“Hii malumbano ya kila siku ya kisiasa inafaa kusitishwa na viongozi kuwasaidia wakenya wanahitaji kufanyiwa maendeleo badala ya kuzozana kila siku, mimi sioni ikisaidia wakenya,” alisema Mudavadi.

Mudavadi baadaye alielekea katika kaunti ya Kwale kwa ziara yake ya siku tatu kukutana na wanachama katika kuandaa mikakati ya kukiimarisha chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2017.