Share news tips with us here at Hivisasa

Licha ya viongozi wa wanafunzi wa chuo cha anuwahi cha Mombasa kupatiwa barua za kufukuzwa chuoni, viongozi hao wameapa kuendelea kupigania haki za wanafunzi na kusema kuwa watangoja suluhu watakapoenda kuwasilisha lalama zao mbele ya kamati ya nidhamu ya chuo hicho tarehe 16 mwezi huu.

Kulingana na rais wa wanafunzi Ocharo Desmond, ambaye aliongea na mwandishi habari huyu siku ya Jumatatu baada ya kuhudhuria mkutano uliowakutanisha na kamati teule kutoka bunge la Kaunti ya Mombasa, wao kama viongozi na wanafunzi kwa jumla hawana makosa, na ni jukumu lao kuwatetea wanafunzi ili kupata haki.

Kiongozi huyo alishangaa ni vipi usimamizi huo uliweza kuafikia uamuzi wa kuwapa barua za kuwakomesha kuenda chuoni hata bila kuwahusisha kwenye mjadala wa kujua kutoka kwao kilichojiri baada ya mgomo wa wanafunzi hao. 

Aidha, alitoa madai kuwa hawana makosa na watatoa ukweli wao mbele ya kamati ya nidhamu ya shule hiyo.

Miongoni mwa viongozi hao ambao walipokezwa barua hizo ni pamoja na Desmond Ocharo, rais wa wanafunzi, Dennis Oseko, ambaye ni naibu wa rais, Caleb Orem naibu wa kiongozi wa masuala ya elimu miongoni mwa wengine.

Ikumbukwe barua hizi zimetolewa baada ya madai kuzuka kuwa viongozi wa wanafunzi ndio waliohusika kuwachochea wanafunzi wengine kudinda kurudi chuo hapo jana ilivyoamuliwa na chuo hicho kufuatia kufukuzwa mwezi jana.