Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amewakosoa viongozi wa kisiasa kwa kutoa matamshi ya chuki na uchochezi, huku akisema kwamba hatua hiyo huenda ikazua mtafaruku.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Abdulswamad alisema kwamba hatua ya kuonyeshana ubabe wa kisiasa hadharani na kutoa matamshi ya chuki inafaa kusitishwa mara moja ili kuepukana na mgawanyiko.

Abdulswamad alisema kwamba viongozi wanafaa kuwaunganisha wakenya kwa kueneza amani, uiano na utangamano na kuachana na siasa za chuki, dini wala kikabila zinazolenga kuzua migawanyiko baina ya wakenya huku akisema kwamba hatua hiyo huenda ikachangia maafa.

Aidha amewahimiza wakenya kuwa waangalifu na viongozi kama hao na kujitenga nao ili kuzidi kudumisha amani katika taifa hili, huku akisema kwamba wakati wa kampeni za siasa haujafika bali viongozi wanafaa kuwatekelezea wananchi maendeleo.

"Viogozi wa kisiasa wanafaa kukoma mara moja kutoa matamshi ya chuki na uchochezi kwani hatua hiyo huenda ikazua tena migawanyiko na, badala yake wawaunganishe wakenya kwa kuhubiri amani kwa sababu tumepitia mengi kutokana na matamshi ya uchochezi," alisema Abdulswamad.

Mbunge huyo wa Mvita ameitaka idara ya mahakama nchini kutoa adhabu kali dhidi ya viongozi wanaowachochea wananchi na kuzua mgogoro, huku akisema kwamba iwapo hatua za dhararu hazitachukuliwa, basi taifa hili litakumbwa na changamoto kubwa.

Kauli ya kiongozi huyo imejiri baada ya baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi katika mikutano ya hadhara.