Viongozi wa kisiasa wametakiwa kushirikiana na wenzao wa kidini ili kuleta uwiano katika taifa hili.
Wito huo umetolewa na mchungaji Johnson Kamau wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la PCEA Dkt Athur mjini Nakuru.
"Naamini hata viongozi wa kisiasa wana mchango mkubwa na wanafaa kushirikiana nasi wa kidini kwa mustakabali wa taifa," alisema mchungaji Kamau.
Wakati huo huo, ametoa wito kwa wakristo kuzidi kuliombea taifa hili hasa sekta ya usalama. Kwa mujibu wake, iwapo viongozi na wakristo kwa jumla watasimama wima katika maombi, basi baadhi ya changamoto hazitashuhudiwa.
"Jambo moja najua ni kwamba maombi ni muhimu sana na ni silaha katika baadhi ya mambo," akaongeza Kamau.
Vile vile, amewahimiza wazazi kujali maslahi na mienendo ya watoto wao ili wasije wakaingia katika mafunzo ya itikadi kali.
Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya kutokea shambulizi huko El Adde na kusabibisha vifo vya wanajeshi kadhaa wa humu nchini.