Mshirikishi mkuu wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC eneo la Pwani Kazkazini Amina Sudi, amewaonya viongozi dhidi ya kuingiza siasa katika suala la usajili wa wapiga kura.
Akiongea na wanahabari katika mkutano wa hamasa mjini Mombasa siku ya Ijumaa, afisa huyo aliwataka viongozi kutoingiza siasa katika zoezi hilo la usajili, na kutoa wito kwa wale walio na malalamishi kufika katika afisi husika ama vituo vya usajili wa wapiga kura.
“Tunawaomba viongozi kutoingiza siasa katika zoezi la usajili wa wapiga kura kwani hatua hiyo huenda ikasababisha vurugu na kuathiri zoezi hilo. Tume ya IEBC haitakubali hilo kutendeka na watakaopatikana wakikiuka sheria watachukuliwa hatua,” alisema Sudi.
Hivi majuzi, Gavana wa Kaunti ya Kwale Salim Mvuyra alidai kuwa maafisa wa IEBC wanaoendeleza usajili huo wamekuwa wakiwahangaisha wananchi.
Aidha, afisa huyo amewashauri wanaotaka kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura kutembelea vituo vya usajili wa wapiga kura ili wapate huduma hiyo.
Sudi alisema kwamba wangali wanaendeleza hamasa kwa wananchi kuhusu usajili huo ulioingia wiki yake ya pili juma hili.
Alisema kuwa atakayekosa kufanya hivyo kwa muda uliotengwa na tume hiyo basi itakuwa vigumu kwake kuhama kituo kimoja hadi kingine kupiga kura.
Sudi alisema kuwa wakaazi ambao hawatabadilisha vituo vyao watalazimika kusalia katika vituo walivyosajiliwa kama wapiga kura hapo awali.