Wakazi wa Kaunti ya Nakuru wametoa ushauri wao kwa viongozi wa kisiasa na pia wakidini wakiwataka waweze kuwaunganisha wakenya na kusisitiza mwito wa amani, upendo na umoja.
Wakazi hao wamesema kuwa ni mwafaka kumwiga Papa Francis, ambaye alikuwa kwa ziara ya siku tatu hapa nchini, aliyedhihirisha unyenyekevu na kuwajali wengine pasi na misingi yoyote.
Wakazi hao wamewasihi viongozi wa kanisa na wa serikali ya kitaifa na za kaunti wanyenyekee na kuiga mfano wa baba mtakatifu ili waweze kuwatumikia watu ipasavyo.
Aidha, wamewataka viongozi hao wa ngazi mbalimbali kwa ushirikiano na wananchi kudhihirisha uwazi, uwajibikaji kwa ajili ya maendeleo katika taifa hili, ambalo wamelitaja kuwa lenye baraka.
Hii ni baada ya baba mtakatifu kuonyesha unyenyekevu kwa kutangamana na watu wa daraja la chini sawa na kutumia magari yasiyo ya kifahari katika ziara yake ya siku tatu hapa nchini.
Itakumbukwa kuwa ziara ya baba mtakatifu hapa nchini ilikuwa ziara ya kwanza kuzuru Kenya na bara la Afrika tangu alipotawazwa kuwa kiongozi wa kanisa katoliki duniani.
Hata hivyo, ziara ya Papa Francis barani Afrika, ujumbe ukiwa ni amani upendo na umoja na maridhiano, imehusisha mataifa ya Kenya, Uganda na kutamatisha na Jamuhuri ya Afrika ya Kati.