Viongozi wa kisiasa na kidini nchini Kenya wametakiwa kujifunza kutokana na unyenyekevu wa kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Aliyekuwa Mbunge wa Rongai Luka Kigen, amesema kuwa viongozi wa Kenya katika ngazi ya kidini na kisiasa wamejawa na maringo na tamaa.

Akiongea Ijumaa mjini Nakuru, Kigen amesema kuwa unyenyekevu wa Papa unapaswa kuwa funzo kubwa kwa viongozi na kuwataka kutangamana na wananchi wa kawaida kila wakati.

"Viongozi wetu ni watu ambao wanapenda magari makubwa makubwa ya kifahari na hawataki kuwa karibu na watu maskini lakini Papa Francis ameonyesha mfano mwema kwa kutumia gari la kawaida na kutangamana na raia wa kawaida," alisema Kigen.

"Haina haja wako kama viongozi kutembea katika misafara mirefu na walinzi wengi kwa sababu hiyo ni gharama kubwa kwa Wakenya walipa ushuru," aliongeza.

Mbunge huyo wa zamani alisema kuwa itakuwa vigumu kwa viongozi kujua shida za raia iwapo watajitenga nao.

"Hata viongozi wa makanisa utawapata wakitembea na walinzi na magari mengi sana na hii inafanya kuwa kama wasio watu wa kawaida, jambo ambalo hata mwenyezi Mungu hafurahii," Kigen alisema.

"Ujio wa Papa unafaa kuwa na funzo kubwa sana kwa viongozi na watambue kuwa watu wanaowaongoza ni muhimu sana kushinda mamlaka," alisisitiza.