Share news tips with us here at Hivisasa

Visa vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto wasichana vimepungua kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa maswala ya kijinsia, visa hivyo vikiwemo ubakaji wa watoto wanaoenda shuleni vimepungua kwa asilimia arobanne, kutokana na kile wanaharakati hao wametaja kuwa kuimarika kwa kampeini dhidi ya vitendo hivyo katika kaunti ya Nakuru.

Kulingana na mwakilishi mteule wa bunge la kaunti ya Nakuru Esther Njeri, kupunguka kwa visa hivyo ni hatua kubwa ikikumbukwa kwamba eneo la Naivasha lilikuwa likiongoza kwenye visa hivyo.

Njeri amesema kuwa mwaka jana pekee kuliripotiwa visa 25 ikilinganishwa na kisa kimoja pekee kufikia sasa mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari mjini Naivasha siku ya Jumanne, kiongozi huyo ameongeza kuwa juhudi sasa zinalengwa kwa mtoto wa kiume ambaye sasa ameonekana kudhulumiwa, huku visa vingi vikikosa kuripotiwa.

“Tutaendeleza vita hivi mpaka tuhakikishe vinapungua kabisa katika kaunti ya Nakuru na pia taifa kwa jumla, na kwa sasa tutajumuisha mototo wa kiume kwa sababu pia nao wanadhulumia na kulawitiwa,” alisema Bi Njeri.