Visa vingi vya uhalifu kama vile vya mauaji na ubakaji vimehusishwa na utumizi wa dawa za kulevya.
Afisa wa majaribio (probation officer) mjini Nakuru Grace Abukuse amesema baadhi ya wanaotumia mihadarati hutekeleza vitendo vya uhalifu bila kukusudia.
Kupitia kwa mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi huyu siku ya Jumamosi, afisa huyo alisema kuwa idadi kubwa ya visa wanavyovipata na haswa vile vya mauaji bila kukusudia hutokana na watu ambao hukiri kuwa wametekeleza maovu hayo bila kukusudia baada ya kutumia dawa za kulevya.
“Tukiangalia swala la utumizi wa dawa za kulevya na athari ambazo hutokana na utumizi wa dawa hizo, haswaa kwenye Jamii, visa vingi vya uhalifu ambavyo hutekelezwa kama vile mauaji bila kukusudia kwa mara nyingi huhusiana kwa karibu na wale ambao hutumia dawa za kulevya,” alisema Abukuse.
Abukuse aidha alisema kuwa washukiwa wengi hukiri kwamba mihadarati ndio sababu iliyowapelekea kutenda uhalifu.
“Unapozungumza na washukiwa wengi ambao hukabiliwa na makosa kama vile ya ubakaji, utagundua kuwa wao hutumia dawa za kulevya kama vile bangi. Wanapozidi kutumia dawa hizo za kulevya, wao hutekeleza makosa makubwa zaidi,” alisema Abukuse.
Matamshi haya yanajiri huku mwenyekiti wa mamlaka ya kudhibiti pombe na dawa za kulevya Nacada John Mututho akionya vijana dhidi ya kujihusisha na utumizi wa mihadarati na pombe akisema huenda tabia hiyo ikawaadhiri pakubwa katika siku za usoni.