Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa wa elimu katika Kaunti ya Nyamira Ziroma Kinayo amesema visa vya udanganyifu katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE havitashuhudiwa katika kaunti hiyo.

Kinayo alisema mikakati ya usalama imeimarishwa kwa shule zote 581 za Kaunti ya Nyamira huku akiwa na matumaini kuwa kaunti hiyo itafanya vizuri katika mtihani huo wa kitaifa.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne muda mfupi tu baada ya mtihani huo kuanza kote nchini, afisa huyo alisema kuwa mitihani hiyo itakuwa ikifanywa chini ya ulinzi mkali katika kaunti hiyo ili kuzuia visa vya udanganyifu.

“Tulifanya kikao na walinzi wa mtihani huo katika kaunti nzima ya Nyamira kuhusiana jinsi mtihani utalindwa. Ninataka kuwahakikishia wananchi kuwa hakutakuwa na visa vyovyote vya udanganyifu,” alisema Kinayo.

Aidha, afisa huyo aliomba wazazi kuwaandaa wanao mapema ili kufika shuleni na kufanya mitihani wao kwa utilivu bila kuharakishwa.

“Naomba wazazi wawe waangalifu na wawe wakiwaandaa wanao mapema ili waweze kufika shuleni kabla ya mtihani kuanza,” aliongeza Kinayo.