Hali ya wasi wasi imeghubikia kijiji kimoja huko Gilgil baada ya visa saba vipya vya ugonjwa wa kipindupindu kuripotiwa.
Kufuatia kulipuka upya kwa ugonjwa huo katika kijiji cha Kasarani Gilgil, maafisa wa afya wamekita kambi eneo hilo ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo.
Visa hivyo vimegundulika eneo la Kosovo ambalo ni makazi ya maelfu ya wafanyikazi wa kampuni za maua.
Hayo yanajiri mwezi mmoja tu baada ya visa 12 vya ugonjwa huo kuripotiwa Gilgil, huku wengi wa waadhiriwa wakilazwa katika hospitali za mji huo na Naivasha.
Afisa msimamizi wa maswala ya afya katika Kaunti ya Nakuru Samuel King’ori amedhibitisha kuwepo kwa maradhi hayo, japo akasisitiza kwamba wamedhibiti hali.
“Tumeweza kuchukua hatua za haraka, na wengi ambao wameadhirika ni wa jamaa moja akiwemo mtoto mchanga lakini wote wameweza kupata matibabu,” alisema Kingori.