Kila kituo cha waendeshaji bodaboda katika Kaunti ya Kisii kimeombwa kusajili waendeshaji bodaboda wake ili kuimarisha usalama.
Hii ni baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya waendesha bodaboda wa sehemu zingine tofauti huja kutoka sehemu zao na kujiunga kwa kituo chochote na kushukiwa kufanya uhalifu.
Akiongea siku ya Jumapili katika uga wa Gusii, Gavana James Ongwae aliomba kila kituo kusajili waendeshaji bodaboda wake ili kuimarisha usalama.
“Ikiwa tunahitaji usalama uwe miongoni mwa wanabodaboda na kutoshukiwa kutekeleza uhalifu, sharti kila kituo kijue idadi ya wanabodaboda kwa kuwasajili,” alisema Ongwae.
“Kuna wanabodaboda ambao huja kutoka sehemu zingine na kujiunga kwa vituo ambavyio sio vyao, hayo mkiendelea kuyakubali huenda muendelee kushukiwa kufanya uhalifu, naomba kila kituo kifanye usajili wa wanabodaboda wake ili kuimarisha usalama,” aliongeza Ongwae.
Mapema siku ya Jumapili, waendeshaji bodaboda katika mji wa Kisii wakiongozwa na Dauglas Obara waliomba maafisa wa polisi kuwaimarishia usalama wao haswa nyakati za usiku, kwa kile walichokisema wanashambuliwa na washukiwa wa ujambazi.
“Tunaomba maafisa wa polisi kufanya ile patroli ya usiku jinsi walivyokuwa wakifanya hapo mbeleni ili kutuimarishia usalama wetu nyakati za usiku,” alisema Obara.