Hatua ya kujiunga upya kwa wanachama wa vuguvugu la Mombasa Republican MRC inaonekana kuwakosesha usingizi viongozi mbalimbali huku wakiwasihi wananchi dhidi ya kuamini propaganda za vuguvugu hilo.
Wakiwahutubia wananchi katika mkutano wa usalama nje ya afisi ya chifu eneo la Kombani, viongozi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa usalama , Evans Achoki wamewatahadharisha wakaazi dhidi ya kuamini propaganda za wafuasi wa baraza la MRC kuwa eneo la Pwani litakombolewa hivi karibuni.
Tahadhari hiyo imetolewa baada ya kubaainika kwamba wanachama hao wanajiunga upya huku wakieneza uvumi kwa wananchi kwamba kuna meli kutoka Uingereza ambayo imetia nanga katika bandari ya Mombasa na inasubiri kuwapatia bendera ya ukombozi.
Aidha mwakilishi wa wanawake Zainab Chidzuga na mbunge wa Matuga Hassan Mwanyoha wamewakashifu vikali wafuasi hao kwa kuwapotosha wananchi kutojisajili kama wapiga kura.
Viongozi hao aidha wamesema kwamba kwa kuwa taifa hili liko katika mfumo wa ugatuzi, basi kuna haja ya baraza la MRC kutupiliwa mbali na kuzikwa katika kaburi la sahau huku wakiwaonya wananchi dhidi ya kujiunga na vuguvugu hilo na badala yake wajiunge na vyama vya kisiasa.