Mwenyekiti wa tume ya mawasiliano katika baraza la maaskofu wa kanisa katoliki hapa nchini Askofu Joseph Obanyi amewahimiza waratibu na mameneja wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kanisa katoliki kuwa katika mstari wa mbele kuangazia maswala ya kanisa.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni askofu wa jimbo katoliki la Kakamega amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari vya kanisa katoliki kuwa na ushirikano baina yao ili kutoa taswira dhabiti kuhusu msimamo wa kanisa katika maswala mbali mbali yanayokumba taifa.
Ameongeza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 unapokaribia, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kanisa katoliki ni sharti viwe katika mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa amani, upendo na utangamano.
Askofu Obanyi aidha amesema kuwa mawasiliano yana nafasi muhimu katika kanisa ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Ameyasema haya Jumatano katika mukutano uliowaleta pamoja waratibu na mameneja wa vitengo vya mawasiliano katika majimbo kuu na majimbo katoliki hapa nchini kenya.
Picha: Mwenyekiti wa tume ya mawasiliano katika baraza la maaskofu wa kanisa katoliki hapa nchini Askofu Joseph Obanyi. Amevihimiza vyombo vya habari kuwa katika mstari wa mbele kuangazia maswala ya amani. amecea.blogspot.com