Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Walemavu wamevipa vyombo vya habari nchini changamoto ya kupea  uzito maswala ya watu wanaoishi na ulemavu, kama njia moja ya kuwaepusha na unyanyapaa.

Walemavu waliozungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru walipendekeza vyombo vya habari kuajiri angalau mlemavu mmoja atakayesaidia kuangazia dhulma za walemavu.

Wakati uo huo, serikali  kuu  imetakiwa  kuyadhibiti  mashirika  mengi yasiyo ya  kiserikali haswa yanayoshugulikia makundi ya walemavu, yakidaiwa mengi yayo yanafisadi walemavu.

Huku siku ya kusherekea walemavu kote duniani ikiadhimishwa siku ya Alhamisi, walemavu katika kaunti ya Nakuru wamesema misaada inayotolewa na wahisani kupitia mashirika hayo haiwafikii hadi mashinani, ila inaishia mifukoni mwa wachache.

Aidha, wamesema hakuna mikakati mwafaka iliyowekwa na serikali kuwapa usaidizi wa moja kwa moja.

“Tunasikia tu mambo ya fedha za uwezo, CDF na zingine, lakini hatusaidiki kwa sababu wanasema tujiunge na kikundi. Je, pesa za kikundi zitatusaidia vipi ilhali wengine hatuwezi kutoka hata kwa viti?” akahoji Dan Mwangi alisema.

Aidha, alipendekeza katika kuyapa makundi ya walemavu fedha za kufanyia miradi, wapewe pesa ambazo zitawawezesha kujiwekea biashara ya kibinafsi.

“Tuache kukumbukwa siku kama ya leo peke yake. Serikali zote gatuzi na ile kuu, ziweke mikakati ya kuwezesha walemavu kote nchini kiuchumi, wao pia wanataka maisha mazuri,” Joram Kamore, anayeshona viatu maili kumi alisema.

Nancy Wanjiru, kutoka kikundi cha Sisterhood, ameitaka serikali kuwatafutia pia soko la bidhaa zao ambazo wanatengeneza, lakini zinaishia kukosa watu wa kununua kutokana na uwepo wa soko tayari la bidhaa hizo.