Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Waalimu katika eneo la Molo pamoja na washikadau wengine wa elimu wameelezea wasiwasi wao kutokana na kisa cha asubuhi ya Jumanne, ambapo genge la wanaume watatu lilijaribu kumbaka msichana wa darasa la nane akienda shuleni.

Mwalimu mmoja wa shule ya Mianzini anakosomea mtoto huyo, alitaka polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kulinda wasichana wengine ambao huenda wakajipata kwenye dhulma sawa na hizo.

“Tulipopata habari hizo tulikimbia kwa kichaka alikokuwa msichana huyo kwa sababu hakuwa anaweza kutembea, kwa vile alikuwa amechapwa miguu. Sare zake zilikuwa na uchafu mwingi, ishara kwamba alijaribu kung’eng’ana nao. Tatizo ni kwamba huenda washukiwa hao wakamkamata mwingine ambaye hana uwezo kama huo,” Mwalimu huyo alisema.

Sasa wazazi wanahofia watoto wao kwenda shuleni asubuhi na mapema, kama washukiwa hao hawatatiwa mbaroni.

Babake mwadhiriwa kwa jina Ayub Wainana amewataka polisi kushika doria kwenye barabara zenye vichaka eneo hilo wakati wanafunzi wakienda shuleni.

“Tunahofia kuharibiwa kwa masomo ya watoto wetu kwa sababu wahuni hao walinuia tu kumbaka msichana wangu," Wainaina alisema.

Aidha alimtaka MCA wa eneo hilo Michael Wang’ombe kuzindua mpango wa kufyeka vichaka vilivyo kando ya barabara.