Waangalizi wa uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi wamesema kuwa shughuli ya upigaji kura katika vituo vyote vilivyopagwa imeanza vyema.
Afisa wa maswala ya Haki na Sheria katika Shirika la Haki Afrika, Francis Auma Gamba amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo mdogo wa eneo bunge la Malindi umefanyika vyema na shughuli ya upigaji kura katika eneo hilo inaendelea.
Auma amesema kuwa usalama wa eneo hilo imeimarishwa kwani maafisa wa usalama wanashika doria kuhakikisha kuwa shughuli ya upigaji kura imefanyika kwa amani bila ya pingamizi zozote licha ya kuwepo na hofu ya kiusalama.
“Tunawaambia wakaazi kuwa shughuli ya upigaji kura imeanza rasmi na tunawahimiza kupiga kura kwa amani na kurudi nyumbani kusubiri matokeo kwani shughuli hii inafanyika kwa njia ya huru na uwazi,” alisema Auma siku ya Jumatatu huku shughuli ya upigaji kura ikiendelea.
Amewahimiza wakaazi kuhakikisha kuwa wanadumisha amani kwa kupiga kura kwa utaratibu na kurudi nyumbani kusubiri matokeo ili kuzuia kushughudiwa kwa vurugu kutokana kwa wafuasi wa wagombea wa kiti hicho.
Kamishna wa Tume huru ya uchauguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC Yusuf Nzibo amewahakikisha wakaazi kuwepo kwa uchaguzi huru na haki huku akiwahimiza waangalizi wa shughuli hiyo kuhakikisha kuwa wanaripoti mara moja tukio lolote lisiloeleweka.