Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu wa rais, William Ruto ametoa hakikisho kwamba serikali itashughulikia maslahi ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Akihutubia wanahabari Ijumaa nyumbani kwake katika mtaa wa Karen tangu kuondolewa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Ruto ameshikilia kwamba waathiriwa wa ghasia hizo zilizoshuhudiwa nchini mwaka 2007/08 wameonyesha uvumilivu na ujasiri katika muda wote ambao wamekuwa wakisubiri haki. Aliahidi kutolegeza juhudi zake hadi pale waathiriwa wote watakapofidiwa. Aidha ameweka wazi kwamba hakuhusika kamwe kupanga au kutekeleza mauaji ya watu na uharibifu wa mali baada ya uchaguzi huo.

"Nasikitika sana kwa yale yaliyotukia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo wengi walipoteza maisha na mali kuharibiwa: kilikuwa ni kipindi cha 'giza' katika historia ya Kenya. Serikali haitachoka katika kuhakikisha kwamba waathiriwa wote wa ghasia hizo wameshughulikiwa ipasavyo," alisema Ruto.

Ruto aidha ametoa wito kwa Wakenya wa tabaka mbalimbali pasi na kuzingatia kabila au dini, kuungana na kuhimiza umoja na utangamano ili kuunda taifa dhabiti.

"Tunastahili kushirikiana pamoja kurejesha umoja wa taifa kwa kuwa wale walioathirika ni sehemu ya taifa la Kenya pasi kuzingatia kabila au tofauti za kidini," aliongeza Ruto.

Mapema mwezi Februari mwaka huu, serikali ilitangaza kutoa shilingi bilioni 1.2 kuwafidia waathiriwa hao huku ikiamrisha kufungwa kwa kambi zote za wakimbizi wa ndani kwa ndani.