Baada ya tume ya elimu ya vyuo vikuu CUE kutangaza kwamba vyuo tanzu vya chuo kikuu cha Kisii vinastahili kufungwa kwa kutoafikia vigezo muhimu, wabunge wawili kutoka kaunti ya Nyamira wamejitokeza kupinga vikali hatua hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakihutubu siku ya Jumamosi, mwakilishi wa kina mama katika kaunti hiyo Alice Chae na mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire walisuta vikali hatua hiyo na kuitaka wizara ya elimu kuingilia kati na kusuluhisha suala hilo. 

"Hili ni jambo la kushangaza sana na ninafikiri kwamba tume ya CUE haijaliangazia kwa uwazi kwa maana tunalozungumzia ni maisha ya mbeleni ya wanafunzi wengi ambao tayari wameathirika na hali hii," alisema Bosire. 

Kwa upande wake, Chae alisema kuwa tume hiyo ilichukua hatua ya kufunga matawi ya chuo cha Kisii kwa haraka na hata bila ya kuwashauri washikadao, hali iliyosema wizara ya elimu nchini inastahili kuingilia kati ili kulinda haki za wanafunzi. 

"Ninaelewa wazi kwamba vigezo wanavyozungumzia tume ya CUE ni mhimu, ila kufungwa kwa matawi kumi ya chuo cha Kisii inamaanisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wataendelea kuathirika zaidi, na ndio maana wizara ya elimu inastahili kuketi pamoja," alihoji Chae. 

Keroka, Nyamira, Kehancha na Eldoret ni miongoni mwa mabewa ya chuo cha Kisii yaliyoathirika na hali hiyo.