Wabunge wa Kaunti ya Nyamira ambao wamekuwa wakishtumu uongozi wa Gavana Nyagarama sasa wamelegeza msimamo wao na kuahidi kumuunga mkono kwenye agenda yake ya maendeleo.
Akihutubu kule Nyamwange siku ya Jumamosi, mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire, aliyewaongoza wabunge wengine watatu alisema kuwa wapo tayari kukutana na gavana Nyagarama ili kujadili jinsi ya kushirikiana kufanya maendeleo kwa kuwa hilo litasaidia pakubwa kutoharibu pesa za umma kurudia kufanya miradi ile ile ya maendeleo.
"Kwa minajili ya watu wa kaunti ya Nyamira, tayari nimewashawishi wenzangu na tumekubaliana kukutana na gavana Nyagarama ili tuweze kujadili maswala yanayoathiri watu wetu, na tutafute njia ya kuyakabili kwa kuwa hilo litatusaidia pakubwa kwa kutumia pesa za serikali ya kaunti na zile za maendeleo ya maeneo bunge CDF vizuri pasina kurudia miradi ambayo tayari isha tekelezwa na gavana ama sisi," alisema Bosire.
Kwa upande wake mbunge wa eneo bunge la Mugirango kaskazini Charles Geni, wakati wakuwa na misimamo mikali dhidi ya uongozi wa gavana Nyagarama umeisha, na alimsihi gavana Nyagarama kuwahusisha wabunge wa eneo hilo ili iwe rahisi kufanya maendeleo kwa wananchi.
"Ni watu wetu wanaoathirika tunapopigana kisiasa. Na kwa kweli tunaweza suluhisha hali hiyo iwapo tutaketi chini na gavana Nyagarama na kufanya mashauriano dhidi ya njia za kusuluhisha tofauti zetu," alisema Geni.
Kwa muda sasa wabunge wa eneo hilo, akiwemo mwakilishi wa kina mama Alice Chae, mbunge wa Mugirango magharibi James Gesami, wa Kitutu Masaba Timothy Bosire na yule wa Mugirango kaskazini wamekuwa wakipinga vikali uongozi wa Gavana Nyagarama kwa kumhusisha na ufisadi.