Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wabunge wa Pwani wamesema kuwa kuna njama katika bunge la kitaifa ya kumuondoa madarakani mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini Mohamed Swazuri.

Akiongea katika mkutano wa harambee huko Tiwi kaunti ya Kwale siku ya Jumapili, mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga alisema Swazuri anafaa kuachiwa uhuru wa kuendesha tume.

“Swazuri apewe nafasi nzuri ya kuweza kufanya kazi yake na asibabaishwe na mtu yeyote,” Gunga alisema.

Kwa upande wake, mbunge wa Mwatate Andrew Mwadime amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchunguza njama hiyo wanayodai inaendelea bungeni.

 “Wanataka kutumia wabunge ili wamtoe Swazuri, tunakuomba rais sisi hatutakubali mapenzi ya danganya toto,” Alieleza Mwadime.

Wabunge hao wanasema viongozi wanaotoka Pwani mara nyingi uwa wanapigwa vita kila wanapopewa fursa ya kusimamia idara au tume ya kitaifa.