Mchanganuzi wa maswala ya kiuchumi Johnson Muchiri amewataka wabunge kuiunga mkono Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchni EACC ili kufanikisha juhudi zake za kuwakabili maafisa wa umma wafisadi.
Kulingana na Muchiri, iwapo wabunge wataendelea kuwapiga vita makamishna wa tume hiyo, basi swala la ufisadi katika afisi mbalimbali za umma litazidi kukita mizizi na kuvuruga shughuli zote za kimaendeleo nchini.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Muchiri alisema kwamba swala la ufisadi nchini limekuwa tatizo sugu na kuchangia serikali kushindwa kumudu gharama za wananchi kutokana na kufujwa kwa mabilioni ya pesa na baadhi ya maafisa wa umma nchini.
Alisema kwamba ipo haja ya wabunge pamoja na viongozi wakuu wa serikali kuiunga mkono tume hiyo kuiwezesha kutekeleza kazi zake vyema, kabla ya taifa hili kuzama katika lindi la umaskini.
Aliitaka serikali kuitengea tume hiyo fedha za kutosha katika kutekeleza majumu yake.
“Sharti wabunge pamoja na viongozi wengine wakuu serikalini kuunga mkono makamishna wa tume ya EACC pamoja na kuitengea fedha za kutosha. Wanapaswa kuiunga mkono tume hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuwakabili maafisa wafisadi badala ya kuipiga vita kila siku,” alisema Muchiri.
Wakati huo huo amemtaka mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko kuidhinisha sheria kali zaidi dhidi ya maafisa wafisadi kama njia moja wapo ya kusitisha kukithiri kwa kashfa za ufisadi nchini.