Vijana kutoka Kangundo, Kaunti ya Machakos, wameshauriwa kuchukua muda wanapochumbiana ili kujuana vizuri kabla ya ndoa.
Akizungumza siku ya Jumatano katika mji wa Kangundo, afisa wa watoto katika eneo hilo, Susan Ouma, alisema kuwa watu wengi huingia katika ndoa kiholelaholela na kutalakiana baada ya muda mfupi, jambo ambalo huathiri watoto kisaikologia.
Afisa huyo alieleza kuwa watoto wengi ambao wazazi wao wametalakiana huathirika sana hasa kimasomo au hujipata mikononi mwa wazazi wa kambo wanaowatesa.
"Naomba vijana wawe waangalifu mno na kuchukua muda kuchumbiana ili kupata kujua mtu unayepanga kufunga pingu za maisha naye,” alisema Ouma.
Aliongeza, “Ni jambo la kusikitisha vijana wanapoamua kufunga ndoa baada ya miezi mitatu ya kuchumbiana, kabla hawajafikia kujuana kiundani kisha baada ya ndoa kunazuka migogoro, ambapo watoto ndio huathirika mno.”
Vilevile afisa huyo alielezea kuwa ndoto ya kila mtoto ni kuwa na familia kamilifu kwani mara nyingi wazazi wanapoachana, watoto hutekelezwa na wengine hutoroka nyumbani au kulelewa na wazazi wa kambo wanaowatesa.