Waendesha bodaboda mjini Kisii wameshauriwa kujiepusha na uhalifu na badala yake kujiunga kwa makundi ambayo yatawafaa kiuchumi na kujiimarisha kimaisha ili kuiendeleza.
Ushauri huo umetolewa baada ya kubainika kuwa baadhi ya waendeshaji bodaboda mjini humo hujihusisha na visa vya uhalifu katika mji huo nyakati za usiku ambapo wanashukiwa kushirikiana na vijana wengine kuwaibia wateja wanaowabeba.
Akizungmza na waandishi wa habari siku ya Juamatano mjini Kisii, mwenyekiti wa polisi jamii mjini humo Stevin Osare aliwashauri waendeshaji pikipiki kujihusisha na masuala ya maendeleo kwa kutumia hela wanazopata kutoka sekta yao uchukuzi na zile za Uwezo Fund kuwekeza kwenye miradi kama ufugaji wa kuku, ufugaji wa samaki na biashara zingine.
Baadhi ya wateja wamekuwa wakilalamika kubebwa usiku na kufikishwa mahala na kunyanganywa bidhaa pamoja na pesa na waendeshaji bodaboda hao.
Imesemekana kuwa waendesha pikipiki huongezeka mjini Kisii usiku ikilinganishwa na wakati wa mchana, huku ikishukiwa wengine hutoka sehemu mbalimbali ili kuwaibia wateja.
“Naomba vijana hawa wa bodaboda, badala ya kuwaibia wateja waanze miradi ambayo itawafaidi kwenye shughuli zao kama ufugaji wa kuku, samaki,kilimo ili kujiendeleza,” alisema Osare.
Osare aidha aliomba vijana hao kukopa pesa ili kuzitumia kwa miradi na kuacha kuogopa kukopa pesa kutoka taasisi za kifedha ikiwa wanahitaji kujiendeleza kimaisha
“Naomba kila kijana awe anawajibika kwa mikopo ili kujiepusha na migogoro na mashirika husika ili kujindeleza,” aliongeza Osare.