Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Waendesha  bodaboda mjini Kisii wamewaomba maafisa wa polisi kuwahakikishia  usalama wao kwani wanahofia kuendeleza shughuli zao za uchukuzi mjini humo.

Hii ni baada ya visa vya kushambuliwa na washukiwa wa ujambazi wasiojulikana kuongezeka katika mji huo haswa nyakati za usiku, ambapo wanajeruhiwa  na kunyanganywa pikipiki zao.

Wakizungumza na mwandishi huyu  siku ya Alhamisi mjini Kisii baada ya waendesha bodaboda hao kumzika mwezao aliyeshambuliwa na majambazi katika barabara ya kutoka mjini Kisii kuelekea Kegati, wanabodaboda hao walisema wamehofia kuendesha shughuli zao hasa nyakati za usiku, na kuhitaji msaada wa usalama kutoka kwa maafisa wa polisi

Evans Oginda, mmoja wa waendesha bodaboda hao alisema visa vya kushambuliwa vimeongezeka, na kuomba maafisa wa usalama kuzidisha doria katika eneo hilo. 

Wiki jana, mwendesha bodaboda mwezao alijeruhiwa katika eneo la Suneka, huku pikipiki yake ikichukuliwa na haijawahi onekana hadi sasa.

“Tunatafutia watoto kupitia sekta hii uchukuzi lakini imefikia mahali wenzetu wanashambuliwa na watu wasiojulikana na kutoroka na pikipiki,” alisema Oginda

"Tunaomba maafisa wa polisi kutuwekea usalama maana penye imefikia tumehofia sana maisha yetu,” aliongezea.