Mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda mjini Kisii Mice Mose amewaomba waendeshaji bodaboda mjini humo kutokubali kutumiwa na wanasiasa, ila kutegemea biashara zao za uchukuzi ili kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha
Ombi hilo limetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya waendeshaji hao mara nyingi ndio hutumika na wanasiasa ambao wanataka kujulikana na kujinufaisha kisiasa na mengine mengi.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, Mose aliwashauri waendeshaji hao kufanya shughuli zao za uchukuzi wakiwa na imani na maono ya kujisaidia katika siku zijazo
“Tumekuwa tukisikia kuwa waendeshaji wengi ndio hutumika kama chombo kwa wanasiasa ambao wanataka kujinufaisha kisiasa, na hiyo ni picha mbaya kwa vijana, kwani sisi tunaonekana kutumika na wanasiasa? wacha tuone jinsi ya kujiendeleza na tujitegemee sisis wenyewe,” alisema Mose
“Naomba kila mwanaboboda kujitegemea na kutokubali kutumika kisiasa ila tu kufikiria jinsi utajiendeleza katika maisha yako binafsi ili kujinufaisha,” aliongeza Mose.
Wakati huo huo, Mose aliwaomba waendeshaji hao wote wa vituo 52 vilioko mjini Kisii kujiandikisha katika vikundi mbalimbali ili kupata mikopo na kujinunulia pikipiki zao kujiendeshea wao wenyewe wala sio kuendesha za wengine.
Mose alisema baadhi ya waendeshaji bodaboda ambao walijiunga kwa vikundi tayari wamenunua pikipiki zao na wamejiendeleza kimaisha, na kutoa ushauri kwa wengine kufanya hivyo ili kupunguza hali ya umaskini.