Waendesha bodaboda katikati mwa mji wa Nakuru wameitaka serikali ya kaunti ya Nakuru kuwajengea vibanda vya kujikinga mvua haswa wakati wa msimu wa mvua kubwa.
Wahudumu hao wamesema kuwa wanalazimika kufunga biashara zao wakati kunapojiri mvua kubwa kwa kuwa hawana mahali pa kujistiri.
Wakiongea mjini Nakuru Uumatatu, walisema kuwa inakuwa vigumu kwao kuwasubiria abiria kwenye mvua na kumtaka gavana Kinuthia Mbugua kuwafikiria hata wao.
Wakiongozwa na wmenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda mjini Nakuru Simon Ongoro,wamesema kuwa kama wapiga kura na walipa ushuru wana haki ya kuboreshewa mazingira yao ya kufanyia kazi.
“Tulipiga kura kama wakenya wengine na tukamchagua Gavana Mbugua na tuna kila haki ya kuitisha huduma kutoka kwake.Sisi tunataka kila stage ya bodaboda ijengewe kibanda cha kujikingia mvua ili tuweze kuwasubiri abiria hata wakati kunanyesha ,”akasema Ongoro.
“Tunalazimika kufunga biashara wakati wa mvua kubwa kwa sababu hatuwezi kuwasubiri abiria kwenye mvua nah ii inafanya kazi kuwa ngumu kwetu na gavana anapaswa kulifikiria swala hilo na kutujengea vibanda,” akasema.
Ongoro aliongeza kuwa kama serikali haina pesa za kuwajengea vibanda hivyo basi wao kama waendesha bodaboda wako tayari kuchanga pesa za kuvijenga.
“Kama hawatajenga basi watuonyesha mahali pa kuvijenga na sisi tutachanga pesa na tujenge,” akasema.