Wamiliki wa pikipiki katika eneo la Likoni wametakiwa kuenda katika afisi za Kaunti ya Mombasa kujisajili na kupewa vibali, ili kupunguza wizi wa mitambo hiyo.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti wizi wa pikipiki kwani itakuwa vigumu kwa wezi kuepa mitego wa polisi, kwa vile vibali hivyo vijawawezesha polisi kubaini mmliki halisi wa pikipiki hizo.
Akizungumza siku ya Jumamosi, mwanakamati wa chama cha wamiliki wa pikipiki katika eneo la Shelly Beach Likoni, Samora Mwula, alisema kuwa vibali hivyo vitasaidia kupunguza visa vya wizi wa pikipiki katika eneo hilo ambavyo vimekuwa vikikithiri kwa siku za hivi karibuni.
Alisema kuwa wezi wa pikipiki wamechukua nafasi ya baadhi ya wamiliki wa pikipiki kukosa vibali hivyo, kuendelea kuiba pikipiki hizo na kuziuza katika kaunti jirani na nchi jirani ya Tanzania.
“Iwapo sisi kama wamiliki wa pikipiki tungechukua vibali kutoka ofisi za kaunti, hatungekuwa tunaibiwa pikipiki zetu. Naomba wenzangu kujisajili kupata vibali hivyo ili isiwe kila mara tunashughulikia kesi za kuibiwa pikipiki katika eneo hili letu,” alisema Mwula.
Haya yanajiri baada ya kuripotiwa visa vingi vya wizi wa pikipiki katika eneo hilo, vinavyotekelezwa na watu wasiojulikana.
Mwula aliiomba serikali ya kaunti kuwasaidia katika harakati za kupigana dhidi ya magenge hayo ya wezi.