Zaidi ya wafanyakazi 1,600 wa kampuni ya kushona nguo ya EPZ iliyooko Changamwe mjini Mombasa walijipata kwenye njia panda siku ya Jumatatu baada ya kufika kazini asubuhi na kupata lango kuu la kampuni hiyo limefungwa.
Wakiongozwa na katibu wao Odongo Otieno, wafanyakazai hao wanadai waliagizwa kuripoti kazini Januari 4, 2015 kutoka likizo, ila walipofika kazini mapema Jumatatu walipata geti imefungwa huku juhudi zao za kutaka kuingia ndani zikigonga mwamba baada ya kuzuiwa na walinzi kwa madai kuwa siku zao za kuhudumia kampuni hiyo zilikuwa zimekwisha.
''Tulifaa kurejea kazini leo ambayo ni Jumatatu tarehe nne, lakini tulipofika hapa tumepata geti imefungwa na pia hatujaruhusiwa kuingia ndani, hii ni njama ya wakurugenzi hawa ya kutaka kutufuta kazi,'' alisema Odongo.
Wafanyakazi hao sasa wanadai wakurugenzi wa kampuni ya EPZ wanalenga kutumia mbinu hiyo ili kuwafuta kazi kufuatia hatua yao ya kujiunga na vyama vya kuwatetea wafanyakazi nchini.
"Kama wanataka kutufuta, watulipe mishahara yetu yote tuende tulipe karo tuwaachie kampuni yao,'' alisema mmoja wao.
Wafanyakazi hao sasa wanamtaka katibu wa chama cha kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini COTU Francis Atwoli kuliingilia kati suala hilo.
Juhudi za wanahabari za kutaka kuzungumza na viongozi wa kampuni hiyo hazikufaulu baada ya walinzi waliokuwa wakilinda geti hiyo kuwazuia kuingia ndani.