Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mamia ya wafanyikazi wa kampuni za maua huenda wasisajiliwe kama wapiga kura kutokana na shajara kinzani na waajiri wao.

Haya yaliibuka wakati wa mkutano ambao uliowaleta pamoja wafanyikazi hao wakiwemo pia baadhi ya wawakilishi wadi siku ya Jumapili, huku ikisemekana kuwa waajiri wao kwa wakati mwingi huwanyima haki ya kushiriki zoezi hilo la kimsingi.

Mwakilishi mteule Esther Njeri alisema kuwa wafanyikazi hao kwa kawaida huondoka kazini saa kumi na moja jioni wakati ambao maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC wanapofunga kazi.

Njeri alisema kuwa eneo la Naivasha lina maelfu ya wafanyikazi wa maua na kuitaka IEBC kuangazia mbinu mwafaka zitakazopelekea kusajiliwa kwao.

“Kwa kawaida mwajiri anafaa kuangalia maslahi ya mwajiriwa maanake pia yeye ana majukumu yake kama mwananchi,” alisema Njeri.

Kiongozi mmoja Antony Rebo naye alisema kuwa shughuli ya usajili wa kura eneo hilo ilikuwa ya chini na kuwataka wakazi wengi kufika kwenye vituo ili kusajiliwa.

“Idadi ndogo ya wakazi wanafika kwenye vituo zote 32 za eneo hili tukio ambalo si la kufurahisha kabisa,” alisema Rebo.