Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyabiashara wa soko la Daraja Mbili mjini Kisii wamelalamikia usambazaji na utumizi wa pesa ghushi maarufu bandia katika soko hilo.

Hii ni baada ya mmoja wa wafanyibiashara wa soko hilo kulaghaiwa shillingi 2,000 na wahuni ambao hutumia pesa bandia kununua bidhaa kutoka kwa mfanyibiashara huyo.

Aidha, wafanyibiashara hao wameiomba serikali kufanya upelelezi na kuwakamata wanaoendeleza utumizi wa pesa hizo bandia.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika soko hilo, wafanyibiashara hao walisema kuna baadhi ya watu wanaoshukiwa kusambaza pesa hizo.

“Tunaomba maafisa wa upelelezi kuanza kufanya msako na wawe wanakuwa hapa soko kila siku ya Jumatatu na Alhamisi ambazo ni siku za soko ili kuwakamata wanaotumia pesa badia,” alihoji Jackline Bosibori, mwanabiashara.

Wafanyibiashara hao walisema wamekadiria hasara kubwa kwa kupewa pesa hizo bandia, na hugundua baada ya wahuni hao kuondoka.

“Wakati wateja wanakuwa wengi, wahuni hupata fursa ya kukukabidhi pesa bandia, wengine wakihitaji tuwape noti za mia moja na kutupatia noti ya 1,000, tunaomba maafisa wa kitengo cha ujasusi kufanya uchunguzi na kuwatia watu hao mbaroni,” alisema Victor Maeba, mwanabiashara mwingine.