Wafanyibiashara wa soko la ‘Market ‘ lililoko katikati ya mji wa kisii wameomba serikali ya kaunti ya kisii kuwapa msaada wa kuwajengea vibanda kwani mvua inayoendelea kunyesha imewasababishia hasara kubwa.
Wakizungumza siku ya Jumanne, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Mary Kerubo na Josephat Ndubi walisema kufuatia mvua inayoendelea kunyesha imeharibu bidhaa zao nyingi na kuomba msaada kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo.
“Tunaomba serikali ya kaunti kutusaidia kwa kutujengea vibanda katika soko letu la Market, ukiona tunaanika na kuanua bidhaa zetu kila siku na bidhaa zingine huharibika,” alisema Mary Kerubo.
Aidha wafanyibiashara hao walisema gavana wa kaunti hiyo James ongwae alipotembelea soko hilo mwezi wa sita mwaka jana aliahidi kujenga vibanda na kuweka maji jambo ambalo halijatimizwa.
“Kila kiongozi anapotembelea wafanyibiashara hutoa ahadi za uongo, gavana Ongwae aliahidi kutufanyie maendeleo hapa sokoni lakini hakuna chochote kimefanywa tunaomba atusaide ,”Josephat Ndubi alisema.