Wafanyibiashara mjini Mombasa wameelezea kufurahishwa kwao kutokana na kuonekana kuimarika kwa biashara kufuatia kuongezeka kwa wageni mjini humo wakati huu wa msimu wa likizo.
Wafanyibiashara hao wakiongozwa na Mwanaisha Ngaree, wamesema kwamba tangu idara ya usalama kuzidisha juhudi zake za kuimarisha usalama mjini humo, biashara zimenoga na kurekodi faida maradufu.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, Mwanaisha alisema kwamba idadi ya wageni mjini Mombasa imeongezeka kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na hapo awali, na hatua hiyo huenda ikaimarisha shughuli zao za kibiashara.
"Tumeona idadi ya wageni ikiongezeka mjini Mombasa na kuchangia biashara zetu kunoga zaidi kwani wateja ni wengi sasa katika masoko yetu ikilinganishwa na hapo awali. Tunatarajia msimu huu wa likizo kutaimarisha uchumi wetu hata kwa asilimia chache,” alisema Mwanaisha.
Hata hivyo, wamiliki wa maduka ya nguo, viatu, vipodozi na mboga wamefurahia kununuliwa kwa bidhaa zao kwa wingi, na kuishinikiza serikali kuwahakikisha wateja wao na wahudumu hao usalama dhabiti ili kufanikisha malengo yao na kuboresha sekta hiyo.
Kwa upande wao wahudumu wa magari ya usafiri pia wamesema kwamba biashara yao imeimarika, huku baadhi ya magari hayo yakipandisha nauli kutokana na wasafiri wanaoelekea maeneo mbali mbali nchini kwa sherehe za mwezi wa Disemba kuongezeka.