Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyibiashara wa maduka na vibanda vya mboga katika eneo la Migadini huko Changamwe wamelalamikia hasara kufutaia wanakandarasi wa kurekebisha mabomba ya maji taka kurundika taka katika malango za maduka hayo.

Wafanyibiashara hao wanadai kuwa kandarasi hiyo ilianza bila ya wao kufahamishwa, hali iliyochangia mazingira duni katika malango ya maduka hayo pamoja na kusambaratisha shughuli za kibiashara.

Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, wafanyibiashara hao, wakiongozwa na Juma Suleiman wamedai kuwa iwapo shughuli kama hiyo inatekelezwa, basi itakuwa vyema kujulishwa ili kutafuta mbinu mbadala za kuendeleza biashara zao zinazowapa pato la kila siku.

"Tunakosa kuelewa ukarabati huo wa mambo ya maji taka jinsi unayotekelezwa kwani umeharibu mazingira na kuchangia kusambaratisha shughuli za biashara," alisema Suleiman.

Kwa upnade wao wahandisi wanaotekeleza kandarasi hiyo wamewasihi wakazi na wafanyibiashara hao kuwa na subra kwani shughuli hiyo inatekelezwa kwa muda mchache.