Afisa wa afya ya umma katika Kaunti ya Nakuru Samuel King’ori amewaonya wahudumu wa bucha na wachuuzi wa vyakula dhidi ya kuwauzia wateja vyakula vilivyoharibika.
Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru siku ya Jumatatu, King’ori alisema kwamba kuna baadhi ya wenye maduka ya kuuza vyakula wanaochanganya bidhaa zilizoharibika na zile nzuri pasi na ufahamu wa wateja wao.
King’ori alisema kwamba ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria inayodhibiti vyakula, dawa na sumu, kifungi cha 254, kuuza bidhaa ambazo muda wake umepita.
Afisa huyo wa afya alisema kuwa watakuwa wakifanya misako ya ghafla katika maduka ya jumla na maeneo ya umma ya kuuzia vyakula ili kuhakikisha vyakula vinavyouzwa viko katika hali bora kwa matumizi ya binadamu.
Haya yanajiri siku mbili baada ya baadhi ya wateja waliouziwa nyama iliyoharibika katika bucha mmoja mjini Nakuru kutoa malalamishi yao kupitia mitandao ya kijamii.
Kufuatia malalamishi hayo, King’ori alifika katika bucha hiyo na kuharibu nyama hiyo ambayo aliitaja kuwa hatari kwa afya ya binadamu.
King’ori alisema atakayepatikana akiuza vyakula vilivyoharibika atakabiliwa kwa mujibu wa sheria, sawa na kufungwa kwa duka lake.