Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kaunti ya Kisii imetakiwa kujenga vyoo katika soko la Kenyenya eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti hiyo.

Wafanyibiashara kwenye soko hilo wamesema kuwa hawana vyoo hali ambayo inazidi kuathiri shughuli kwenye soko hilo.

Wakiongea na waandishi wa habari siku ya Jumapili katika eneo la Kenyenya, wafanyibiashara hao hao walilalamika na kuisuta serikali ya kaunti hiyo kwa madai ya kukosa kuwapa huduma zinazofaa.

“Tunaomba serikali ya kaunti ya Kisii kutujengea vyoo vipya na kujali maisha yetu. Tunasubiri kuona ujenzi huo ukianza kwani sisi hulipa ushuru katika soko hili kama wafanyibiashara," Peter Nyabuto alisema.

Wakati huo huo, wakazi nao walidai kutengwa na serikali ya kaunti haswa kimaendeleo na kuitaka kuhakikisha wanafanya miradi ya maendeleo kwenye eneo bunge hilo.

“Serikali ya kaunti ihakikishe imefanya juhudi za maendeleo kama maeneo bunge mengine ili tuwe sawa kimaendeleo,” Isaiah Migosi alisema.

Sasa ni jukumu la serikali ya kaunti kupitia gavana James ngwae kuitikia wito wa wafanyibiashara hao na wakazi kutekeleza yale wanahitaji wakazi kufanyiwa.