Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii Elijah Moindi amewaomba wafanyibiashara wa soko la Keroka kufanya biashara zao kwa amani na kuasi vurugu za kila mara.

Hii ni baada ya wafanyibiashara hao kuwa na mzozo wa mpaka kujua soko hilo la Keroka liko katika kaunti ipi kati ya kaunti ya Nyamira na kaunti ya Kisii jambo ambalo hupelekea Vurugu kushuhudiwa kila wakati.

Akizungumza siku ya Jumapili katika soko hilo, Moindi aliomba wafanyibiashara hao kudumisha amani akisema yeye na mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire pamoja na magavana wa kaunti hizo mbili John Nyagarama na wa Kisii James Ongwae tayari wamefanya kikao na kukubaliana soko hilo liko chini ya uongozi wa kaunti hizo mbili.

“Hakuna haja kwa wafanyibiara na wakazi kuwa na Vurugu za kila mara hapa Keroka kuzozania mpaka sisi viongozi tulikubaliana kuwa soko hili liko chini ya uongozi wa kaunti mbili,” alisema Elijah Moindi

Wakati huo huo, Moindi aliwakosoa baadhi ya watu ambao wanachangia mzozo huo wa mpaka kuibuka katika soko hilo.

“Wale ambao huchochea ghazia katika soko la Keroka siku zao zinahesabiwa sisi tunahitaji kukaa na kufanya biashara zetu kwa amani ili kuinua uchumi wa kaunti hizi mbili pamoja na uchumi wa kitaifa,” Moindi aliongeza.