Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyibiashara wa soko la Mogonga katika eneo bunge la Bomachoge Borabu wamesusia na kuapa kutotozwa ushuru hadi serikali ya kaunti hiyo ifanye maendeleo katika soko hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumapili katika soko hilo, wanabiashara walisema hakuna ushuru utakusanywa katika soko hilo hadi serikali iwafanyie yale wanahitaji.

Miongoni mwa yale wafanyibiashara hao wanahitaji yafanywe katika soko hilo ni kujenga vyoo vipya, kukarabatiwa kwa soko hilo kuwa la kisasa, kujengwa kwa vibanda vya waendeshaji bodaboda, soko kusafishwa kila wakati miongoni mwa mahitaji mengine.

Wafanyibiashara hao waliwafukuza wakusanyaji ushuru huku wakiwatishia kutoonekana katika soko hilo tena hadi mabadiliko yaonekane.

“Serikali ya kaunti ilituahidi kutujengea soko, vyoo vipya, vibanda vya wanabodaboda na hadi sasa hakuna chochote kimefanywa,” alisema John Omae, mwanabiashara.

“Tumeapa hatutatozwa ushuru na hatutalipa liwe liwalo, maana zile pesa tumekuwa tukilipa kama ushuru tunahitaji zitumike kufanya kazi ili kutimiza ahadi na mahitaji yetu,” aliongeza Omae.

Aidha, walidai kuwa sehemu hiyo ya Bomachoge imekuwa ikibaguliwa na serikali ya kaunti, wakidai idadi kubwa ya masoko katika kaunti hiyo zimekarabatiwa huku yao ikisahaulika kwa muda mrefu.