Wafanyibiashara wa soko la Itibo katika eneo bunge la Bobasi, kaunti ya Kisii waliandamana kulalamikia hali mbaya ya soko lao kwa kile walichokisema ni kutokarabatiwa kwa soko hilo kwa muda mrefu.
Wafanyibiashara hao waliandamana siku ya Jumanne katika barabara za eneo hilo huku wakiapa kutotozwa ushuru hadi serikali ya kaunti ifanye yale wanahitaji yafanywe katika soko hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika eneo hilo la Itibo walipokuwa wakiandamana, wafanyibiashara hao walisema hakuna vyoo katika soko hilo, mazingira mabaya, kutokarabatiwa kwa soko, ukosefu wa kiwanja cha kutupa taka miongoni mwa mengine na kuapa kutotozwa ushuru hadi kaunti ishughulikie hayo yote kikamilifu.
Wakati huo huo, wafanyibiashara hao waliporudi kwa soko lao waliwafurusha watoza ushuru na kuapa kuwa hawatalipa hadi mahitaji yao yashughulikiwe.
“Ushuru ambao tumekuwa tukitoa ilikuwa inaenda wapi na soko letu likiwa katika hali hii? tunasema hakuna ushuru itatolewa kwa soko letu hadi serikali ya kaunti iingilie kati na kutufanyia maendeleo kama soko zingine,” alisema Julius Nyangenya, mfanyibiashara mwingine.