Share news tips with us here at Hivisasa

Kamati ya biashara na vyama vya ushirika katika bunge la kaunti ya Uasin-Gishu imesema masoko mawili ambayo yalijengwa kwa kima cha milioni 27 hayanufaishi wafanyibiashara lengwa.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Peter Chomba, ilisema Jumatatu hii kuwa masoko hayo ambayo yalijengwa kupitia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia hayaletei kaunti ya Uasin-Gishu faida yeyote kama ilivyotarajiwa.

Kukosekana kwa faida kutoka kwa masoko hayo kunatokana na hatua ya wafanyibiashara lengwa kususia masoko hayo, wakidai kuwa yako mbali na wateja wao hivyo basi hayatumiki kama ilivyokusudiwa.

Masoko hayo ni soko la Huruma na Kapseret ambayo yako viungani mwa mji wa Eldoret.

Uliokuwa utawala wa manispaa ya Eldoret ulikusudia masoko hayo kutumiwa kupunguza msongamano wa wachuuzi katikati mwa mji wa Eldoret.

Licha ya wazo hilo kukumbatiwa na utawala wa sasa wa kaunti, bado masoko husika hayatumiki kama ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, Chomba alitaka utawala wa kaunti hiyo kushirikiana na wadau wote katika sekta ya biashra ili kubuni mbinu mbadala ya kuona kwamba masoko hayo yanatumika vilivyo.

“Iwapo tutanyamaza, masoko haya yataendelea kuwa mahame ilhali ni raslimali ya umma ambayo inapaswa kuletea kaunti faida, tunapaswa kushirikiana ili kutafuta mbinu ya kochochea matumishi ya masoko haya ili kuletea kaunti mapato,” alisema Chomba.