Wafanyibiashara wa soko la Daraja Mbili mjini Kisii wametishia kuandamana ikiwa serikali ya kaunti haitajenga vyoo vipya katika soko hilo kwa mwezi mmoja ujao.
Hili linajiri huku wafanyibiashara hao wakisema wamelalamika kwa muda mrefu, jambo ambalo limewakera wengi na kutoa makataa ya mwezi mmoja kuandamana ikiwa jambo hilo halitashughulikiwa kikamilifu.
Kulingana na wafanyibiashara hao, vyoo ambavyo serikali ilijenga hapo mbeleni havitoshi kwa soko hilo kwani ni vichache, na husababisha msongamano kwani soko hilo linawabeba wafanyibiashara wengi zaidi haswa siku ya Jumatatu na Alhamisi.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku Alhamisi katika soko hilo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Edward Bosire na Naftal Ombae walisema serikali ya kaunti imekuwa ikiombwa kwa unyenyekefu kujenga vyoo vipya kwa muda mrefu, lakini ombi lao halijawai itikiwa.
“Tunaomba serikali ya kaunti ya Kisii kutujengea vyoo vipya katika soko letu na viwe vyoo vya kutosha maana tunashuhudia msongamano mkubwa kwa vyoo vile ambavyo viko kwa sasa,” alisema Bosire.
“Baada ya mwezi mmoja kukamilika tutaandaa maandamano kulazimisha serikali ya kaunti kutujengea maana imeonekana kuwa tusipoandamana hakuna suluhisho,” alisema Naftal Ombae mwanabiashara mwingine.