Wafanyikazi wa serikali ya Kaunti ya Kisii wamehimizwa kujitenga na masuala ya kisiasa na kufanya kazi waliyoajiriwa kuifanya.
Ushauri huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wafanyikazi ambao wanaitumikia serikali ya kaunti hiyo na tayari wamejiingiza katika mambo ya kisiasa na kusahau kile walichoajiriwa kufanya .
Akizungumza siku ya Jumamosi katika uwanja wa Gusii wakati wa kusherekea siku kuu ya Jamuhuri, mwenyekiti wa chama cha walimu KNUT katika kaunti ya Kisii Geoffrey Mogire aliwashauri wafanyikazi wa kaunti hiyo kufanya kazi na kujitenga na siasa ikiwa wanahitaji gavana wa kaunti apate fursa ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao.
Kulingana naye, kuna baadhi ya wafanyikazi wa kaunti hiyo ambao wameanza siasa za kupotosha, na kusahau walichoajiriea kukifanya.
“Wafanyikazi wa kaunti hii, wale mliajiriwa hamna kibali cha kupiga au kuleta siasa katika kaunti hii, mliajiriwa ili kufanya kazi na kuitumikia serikali ya kaunti hii,” alisema Mogire.
“Wale wafanyikazi wa kaunti wanaofanya siasa mkiendelea kufaya siasa hiyo huenda mbadilishe uongozi wa kaunti, nawaomba mjaribu kujitenga na siasa na kufanya kazi ambayo italeta Maendeleo,” aliongeza Mogire.
Ata hivyo, mwenyekiti huyo alisema gavana Ongwae atachaguliwa kupitia ile kazi wafanyikazi wake wameifanya na kumwomba gavana kuagiza wafanyikazi wake kuacha siasa na kufanya kazi ambayo itamsaidia kuchaguliwa tena.