Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wafanyakazi 400 wa mamlaka ya maendeleo Pwani waliandaa mgomo wa amani siku ya Jumatano wakiulalamikia mshahara wa miezi minne ambayo wanadai hawajalipwa.

Kwa mujibu wa kiongozi wao Bi Fatuma Ali Daba, wafanyikazi hao wamelazimika kususia kazi na kuandamana baada ya ilani ya siku 14 waliyowapa waajiri wao kutamatika bila kupewa majibu.

"Tuliwapa ilani ya majuma mawili lakini wamesalia kimya hadi sasa, hawajatupigia simu wala kutuma barua kutuarifu mbona hadi sasa hatujalipwa mshahara," alisema Bi Fatuma.

Kulingana na mmoja wao aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa, wanadai kuwa pia hawajalipwa marupurupu ya miezi mitatu, na sasa wanamtaka mkurugenzi James Mwangi, aachishwe kazi kwa kile wamekitaja kama kushindwa kuwajibika.

Aidha, wameapa kutorejea kazini hadi malalamishi yao yatakapo sikizwa na kutatuliwa.

"Haturudi kazini hadi watulipe, wakikataa kutulipa tutaelekea mahakamani kutafuta haki," alisema Bi Farida.

Hadi tukiandika taarifa hii, mkurugenzi wa mamlaka hiyo, James Mwangi, ambaye hakuwa afisini wakatai wa mgumo huo, hajatoa taarifa zozote.