Huenda wafanyikazi wa umma katika kaunti ya Nyamira wakajipata matatani iwapo pendekezo la mwaniajia mmoja wa kiti cha uwakilishi wa kina mama litaidhinishwa na bodi ya uajiri wa wafanyikazi wa umma katika Kaunti ya Nyamira.
Akihutubu kule Nyansiongo siku ya Jumanne mwanasiasa huyo, Annet Onsando, alisema kuwa wafanyikazi wengi wa umma wamekuwa walijihuzisha pakubwa na masuala ya siasa, ambayo ni kinyume na sheria za utendakazi wa wafanyikazi wa umma.
Sheria za utendakazi wa wafanyikazi wa umma ni wazi na kama mwananchi anayezingatia sheria sitasita kuwaripoti maafisa wanao jihuzisha na masuala ya siasa, na tayari kuna wale ambao wangali wanachunguzwa dhidi ya madai yakuwawakilisha wanasiasa kwenye hafla za kisiasa," alisema Onsando.
Onsando aidha alihoji kuwa baadhi ya wabunge wa bunge la kitaifa na wale wa mabunge ya kaunti wamekuwa na mazoea ya kuwatuma maafisa wa serikali kuwawakilisha kwenye hafla za umma, hali aliyosema inaweza kuthibitiwa iwapo serikali ya kaunti hiyo itaanzisha mpango wa kuwakagua kila siku wafanyikazi wake wanao ripoti kazini.
"Hili sio jambo geni kusikia kuwa baadhi ya wabunge wa bunge la kitaifa na hata pia wawakilishi wadi wamekuwa wakiwatuma marafiki zao ambao ni wafanyikazi wa umma kuwawakilisha kwenye hafla za michango, na hili haliwezi ruhusiwa na ndio maana inafaa serikali ya kaunti hii kuchukua hatua," aliongeza Onsando.