Mkuu wa idara ya barabara na kazi za umma kwenye Kaunti ya Nyamira Janet Komenda amewaonya wafanyikazi wa kaunti walio na mazoea yakuiba mafuta ya gari za idara hiyo.
Akiwahutubia wafanyikazi hao nje ya afisi za idara hiyo siku ya Jumatano Komenda alisema kuwa mfanyikazi yeyote atakaye patikana akishiriki wizi huo wa mafuta ya gari za umma atafutwa kazi mara moja na kisha nafasi zao kutangazwa.
"Matumizi ya mafuta kwenye idara hii ni yakushangaza na kamwe siwezi kubali kila mara kuitwa na mwajiri wangu kujibu maswali ya matumizi mabaya ya mafuta, ilhali wahusika wako miongoni mwenu. Yeyote atakaye patikana atafutwa kazi mara moja na nafasi yake kutangazwa kuwa wazi," alisema Komenda.
Komenda alisema kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa ili kubaini wafanyikazi wanao iba mafuta ya diseli na watakao patikana kuhusika watatajwa hadharani ili kuwa funzo kwa wengine.
"Ningependa kuwajulisha kuwa tungali tunawachunguza baadhi yenu kwa kuwa idara hii imekuwa ikipoteza lita kadhaa za mafuta ya diseli kwa njia ya wizi. Hilo kamwe halitaruhusiwa na tutawataja hadharani wahusika pindi tu uchunguzi utakapo kamilika," alisema Komenda.
aya yamejiri baada ya kamati ya uwekezaji na uhasibu wa pesa za umma kumhoji Komenda juu ya matumizi mabaya ya fedha kwenye wizara yake mapema wiki hii.